Na Sarah Pelaji
HAYA njoni tusemezane mazingira mali yetu, uhai wetu na fahari yetu. Tulirithituwarithishe. Tulipewa bure tuwape bure.
Kwa maneno hayo tangulizi sichelei kuikumbusha jamii maneno ya Mwenyezi Mungu alipoumba ulimwengu “ Tazama Mungu Aliumba mbingu na nchi …..kia alichokiumba tazama ni chema …. Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu akamweka katika bustani ya Edeni ailime na kuitunza,’ Mwanzo 1-2.
Kumbe misitu, wanyama, mito na viumbe vyote mwanadamu alipewa na Mungu ili avitawale apate mahali salama pa kuishi. Mwanadamu hakununua mazingira bali alipewa bure. Mazingira yaliipendezesha bustani ya Edeni, mazingira yanapendezesha dunia.
Mazingira ni Baraka na ni uhai wa mwanadamu na kila kiumbe kilichoko hai. Hivyo ni wajibu wetu kuyatunza kwani ni agizo la Mungu.
Kadri siku zinavyopita ulimwengu unabadilika na watu wanabadilika. Kibaya zaidi mwanadamu amebadilika na kuwa chanzo cha taabu kwake mwenyewe na kwa viumbe vilivyo hai kwa kuharibu mazingira ambayo ni makao ya viumbe hivyo.
Kuharibu mazingira kutokana na shughuli za mwanadamu zimekuwa ni sehemu ya maisha. Ndiyo maana mwanadamu anafyeka miti ili apande ukoka wa kupumzikia, atengeneze eneo la kuogelea, akijua ndiyo maana ya kutawala ulimwengu.
Mwanadamu anakata miti ili ajenge nyumba, anachimba katikati ya mto ili apate madini, anakata mti apate mkaa wa kupikia ama afanye biashara nk.
Tatizo kubwa linakuja pale mwananchi wa kawaida anapoona kuwa kupanda miti ama kutunza mazingira ni kazi ya serikali. Msitu ukiungua moto, ukigeuzwa jangwa mwananchi anaona hasara ni ya serikali. Hapo ndipo tatizo lilipo.
Ndiyo maana serikali na wadau wa mazingira wanafanya jitihada mbalimbali ili kunusuru dunia na janga hili la uharibifu wa mazingira ikiwemo kukata miti hovyo.
Ikumbukwe kuwa serikali kupitia Wizara ya Mali Asili na Utalii Idara ya Misitu na Nyuki imetoa mwongozo rahisi wa usimamizi wa Misitu kwa pamoja ikihamasisha kuwa, kazi ya kulinda misitu si ya serikali tu bali ya jamii nzima.
Ndiyo maana Kampeni ya Mama Misitu kwa niaba ya Idara ya Misitu na Nyuki inahamasiha jamii usimamizi shirikishi wa misitu kwa pamoja yaani mmiliki mmoja wa msitu yaani serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo wanakijiji wanaoishi karibu na msitu husika.
Aidha jamii inatakiwa ifahamu jukumu la kusimamia misitu yao kwani msitu ukiteketea kwa moto, wananchi wakakata miti kukabakia jangwa hasara si ya serikali tu bali ni ya jamii nzima hususani ile inayoishi karibu na misitu hiyo.
Pia mwongozo huo wa Oktoba 2015 unaeleza misingi minane muhimu kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Misitu kwa pamoja ikiwa ni pamoja na; Jamii kama wasimamizi/mameneja
wa misitu; Hii ikimaanisha kuwa, usimamizi shirikishi wa misitu unahamasisha jamii zinazopakana na misitu kuwajibka katika usimamizi wa misitu kwa kulinda msitu na kufanya doria. SOMA ZAIDI